Wiper wamtaka Raila kumchagua Kalonzo kuwa naibu wake

Muhtasari

• Viongozi  wa Wiper wanamtaka Raila kumchagua Kalonzo kuwa naibu wake.

• Wamesema kwamba Kalonzo alipaswa kuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya ila akakatiza azma yake kumuunga Odinga Mkono.

Viongozi wa chama cha Wiper sasa wamempa Raila Odinga masharti ya kumchagua Kalonzo Musyoka kama naibu wake mbele ya uchaguzi mkuu mwezi Agosti.

Kulingana nao, Kalonzo ndiye aliyepaswa kuwa rais wa tano wa Kenya ila akasitisha azma yake ili kumuunga Odinga mkono.

Wanaamini kwamba kupewa wadhfa wa unaibu rais ndo zawadi ya pekee ambayo inaweza kuendana na kitendo chake cha uzalendo.

Walimtaja kuwa kiongozi mwenye uzoefu na tajriba kubwa ya kuliongoza taifa hili.

Kwa upande wake Kalonzo alisema kwamba swala la naibu wa Raila halipaswi kuwa changamoto kwani anajua atapewa nafasi hiyo.

Aidha, alishikilia kwamba atapambana kisawasawa katika mchakato wa kuuza sera za Raila Odinga na Azimio la Umoja One Kenya Alliance kwa ujumla. 

"Nilisema nitamuunga mkono Raila Odinga, na wale wananijua mimi sirudi nyuma," Kalonzo alisema.

Huku hayo yakijiri, magavana Alfred Mutua, Kivutha Kibwana na Charity Ngilu sasa wanataka makubaliano yao na vuguvugu la Azimio kuangaliwa tena kwa kile wanachokitaja kuwa maslahi yao kutoshughulikiwa.