(VIDEO) Mwanasiasa azidiwa hisia,atiririkwa na machozi kwa kuchangiwa pesa za kampeni

Dr. Mutai Erick Kipkoech
Dr. Mutai Erick Kipkoech
Image: Facebook

Erick Mutai, mwanasiasa anayelenga kugombea ugavana Kericho kwa tiketi ya chama cha naibu rais, UDA alizidiwa na hisia za kitendo cha wananchi kuamua kumchangia hela za kampeni yake na mpaka kufungulia mifereji ya machozi yake hadharani.

Katika tukio hilo lililofanyika Jumamosi iliyopita katika moja ya kampeni zake, Mutai aliwaambia wananchi wake kwamba tofauti na wagombea wenza wenye magunia ya hela za kumwaga katika kampeni zake, yeye kwake hali ilikuwa banu wa sakanu na kuwataka kwa moyo mkunjufu wamfadhili kwa hela za kampeni za mchujo wa chama cha UDA zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Aprili ambapo Mutai anawania tiketi ya chama hicho na aliyekuwa Waziri wa ugatuzi Charles Keter.

Alishangazwa sana na ishara ya wananchi waliojitolea vikubwa na vidogo kumchangia hela za kiasi kikubwa kisichojulikana, jambo lililolegeza macho yake na kujipata anatiririkwa na machozi ya furaha pasi na kuamini ishara hiyo ya wananchi.

Kitendo hiki kilizua gumzo mitandaoni kwa kuwa kilionekana kuenda kinyume kabisa na kawaida ya mkutadha wa kisiasa ambapo kwa kawaida wanasiasa ndio hutoa pesa kwa wananchi kwa kuwahonga kwa kura zao lakini safari hii wananchi ndio walitoa pesa kwa mwanasiasa kwa kufadhili kampeni zake.

Furaha iliyoje mabibi na mabwana!