Jaguar ateta baada ya kubwagwa katika mchujo wa UDA, Starehe

Muhtasari

• Mbunge wa Starehe Charles Njagua almaarufu  'Jaguar' amepata pigo kubwa baada ya mpinzani wake kukabidhiwa tiketi ya UDA kuwania kiti cha Ubunge Starehe.

• “Watu wa Starehe walinyimwa haki yao ya kidemokrasia ya kwenda kupiga kura tena kwa uteuzi na kuchagua kiongozi wao. Chama kiliamua kufanya kura za maoni ili kuamua ni nani wa kukabidhi cheti cha uteuzi na imefanyika,” Njagua alisema.

Charles Njagua
Charles Njagua
Image: Instagram

Mbunge wa Starehe Charles Njagua almaarufu  'Jaguar' amepata pigo kubwa baada ya mpinzani wake kukabidhiwa tiketi ya UDA kuwania kiti cha Ubunge Starehe.

Njagua ambaye alikuwa akichuana na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Simon Mbugua alishindwa katika kura za maoni zilizofanyika Jumatano.

Starehe ilighairi uchaguzi wao wa mchujo wa UDA wiki jana kutokana na kile kilichotajwa kuwa masuala ya usalama.

Inaaminika kuwa wafuasi wa mbunge wa Starehe Njagua na mpinzani wake mbunge Simon Mbugua walikabiliana  na kusababisha kuahirishwa kwa zoezi hilo.

Bodi ya kitaifa ya uchaguzi ilitangaza kuwa chama hicho kitatumia kura za maoni ili kuwatambua wagombea maarufu na wenye ushawishi.

 Lakini Njagua ameteta kuwa wapiga kura wake walinyimwa haki yao ya kidemokrasia ya kwenda kupiga kura na kuchagua kiongozi wao.

“Watu wa Starehe walinyimwa haki yao ya kidemokrasia ya kwenda kupiga kura tena kwa uteuzi na kuchagua kiongozi wao. Chama kiliamua kufanya kura za maoni ili kuamua ni nani wa kukabidhi cheti cha uteuzi na imefanyika,” Njagua alisema.

"Je, hii inaweza kuwa matokeo ya vyeti vilivyokuwa vinazungumziwa kabla ya uteuzi? Je, demokrasia iko hatarini hapa?" aliuliza.

Mbunge huyo aliyemaliza muda wake alisema atafanya majadiliano na wananchi wa Starehe na kuamua atafanya uamuzi gani kwenda mbele.

Njagua alijiondoa rasmi katika chama cha Jubilee na kujiunga na chama cha Naibu Rais William Ruto mapema Januari mwaka huu.

Kabla ya hapo, alikuwa amezunguka nchi nzima na Ruto, ambaye anatafuta kuwa Rais wa tano wa Kenya.

Mnamo 2017, aliwania kiti cha ubunge cha Starehe kwa tikiti ya Jubilee na akashinda.

Alipata kura 52,132 na kufuatiwa na Steve Mbogo wa Orange Democratic Movement (ODM) aliyepata kura 32,357. Mwanaharakati Boniface Mwangi ambaye pia alikuwa kwenye kinyang’anyiro hicho alipata kura 13,413.