Raila na Ruto kukutana na Chebukati Jumatano

Muhtasari

• Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imewaalika wagombeaji urais kwa mkutano wa mashauriano kuhusu sajili ya wapiga kura. 

• Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliwaidhinisha wagombeaji wanne wa urais na kutupilia mbali maombi ya wagombeaji wengine 13 ambao walikuwa wamewasilisha stakabadhi zao. 

MWENYEKITI WA IEBC WAFULA CHEBUKATI
Image: EZEKIEL AMING'A

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imewaalika wagombeaji urais kwa mkutano wa mashauriano kuhusu sajili ya wapiga kura. 

Katika barua iliofikia meza yetu ya habari, mkutano huo utafanyika Jumatano Juni 29, katika Hoteli ya Windsor Golf na Country Club.

 "Tume inakualika kwa mkutano wa mashauriano wa wagombea urais ulioratibiwa kufanywa Jumatano tarehe 29 Juni 2022 katika Hoteli ya Windsor Golf na Country Club kuanzia saa tatu asubuhi," barua hiyo ilisema. 

Baadhi ya mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na daftari lililochapishwa la wapiga kura, njia ya matokeo ya uchaguzi na kuainisha ratiba za kampeni za wagombea urais. 

"Tafadhali kumbuka kuwa unaweza kuandamana na watu wasiozidi watano kwenye mkutano." 

Mkutano huo unafuatia wasiwasi wa baadhi ya wadau kuhusu uamuzi wa tume ya IEBC kutumia mitambo wa kidijitali pekee kuwatambua wapiga kura.

Tume ya IEBC imetakiwa kueleza mfumo mbadala wa kuwatambua wapiga kura ikiwa mitambo ya dijitali itafeli.  

Tume hiyo ilikuwa imeeleza kuwa matumizi ya sajili kwenye daftari ni baadhi ya sababu zinazochangia pakubwa udanganyifu katika shughuli za upigaji kura.  

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliwaidhinisha wagombeaji wanne wa urais na kutupilia mbali maombi ya wagombeaji wengine 13 ambao walikuwa wamewasilisha stakabadhi zao. 

Wanne walioidhinishwa ni kinara wa Azimio Raila Odinga na mpinzani wake mkubwa William Ruto wa chama cha UDA. 

Wengine ni kiongozi wa Chama cha Agano David Mwaure Waihiga na Prof George Wajackoyah wa Roots Party. 

"Wagombea hao walitimiza mahitaji ya kikatiba na kisheria, na hivyo wakafaulu katika azma yao ya kuwania," Chebukati alisema.