Uganda sasa inachunguza shahada ya Johnson Sakaja

Uchunguzi huo unafuatia barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI)

Muhtasari

•Kupitia kwa  Mkurugenzi Mtendaji wa NCHE Mary Okwakol, alisema taasisi hiyo iko katika hatua ya juu ya uchunguzi na kutoa ripoti yao karibuni.

•Serikali ya Uganda imeanza kuchunguza cheti cha shahada kilichotolewa na Chuo Kikuu cha Timu kwa Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Johnson Sakaja,baada ya kujiwasilisha katika makao makuu ya DCI
Johnson Sakaja,baada ya kujiwasilisha katika makao makuu ya DCI
Image: RADIO JAMBO

Serikali ya Uganda imeanza kuchunguza cheti cha shahada kilichotolewa na Chuo Kikuu cha Team kwa Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Kulingana na gazeti la Uganda la New Vision, Baraza la Kitaifa la Elimu ya Juu (NCHE) limethibitisha kuwa lilikuwa likichunguza Chuo Kikuu cha Team kuhusu shahada ya Bw Sakaja.

Kupitia kwa  Mkurugenzi Mtendaji wa NCHE Mary Okwakol, alisema taasisi hiyo iko katika hatua ya juu ya uchunguzi na kutoa ripoti yao karibuni.

“Tukimaliza uchunguzi wetu, kila mtu atajua. Hatuwezi kushiriki chochote sasa hadi uchunguzi ukamilike,” Prof Okwakol alisema.

Uchunguzi huo unafuatia barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa Waziri wa Elimu na Michezo wa Uganda Janet Museveni, ambaye pia ni mke wa rais, akiiomba serikali ya Uganda kuchunguza kukabidhiwa shahada hiyo kwa Bw Sakaja.

DCI ilianza uchunguzi kuhusu uhalisi wa shahada hiyo baada ya kushuku kuwa cheti cha shahada hiyo huenda kilitolewa kwa njia ya udanganyifu. Wiki jana, Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu nchini Kenya (CUE) iliondoa barua ya kubatilisha utambuzi wa cheti cha shahada ya Bw Sakaja.

Hii ilikuwa baada ya Bw Sakaja kuwasilisha kesi ya kudharau mahakama akiishtumu kwa kukosa kuondoa barua hiyo.

Awali CUE ilimtaka Bw Sakaja kutoa kitambulisho cha mwanafunzi wake wa Chuo Kikuu cha Team, barua ya kujiunga, nakala ya orodha ya wahitimu, picha ya kuhitimu na ushahidi mwingine wowote, kuonyesha kwamba alihudhuria masomo na kufuzu katika chuo kikuu.

Gazeti la The New Vision limeripoti kuwa, ingawa Chuo Kikuu cha Team hakikujibu maswali kuhusu uhalisi wa shahada ya Bw Sakaja, mahojiano na mwanafunzi wa zamani yalifichua kuwa Bw Sakaja hakuwa miongoni mwa wanafunzi waliofuzu na shahada ya Sayansi katika Usimamizi mnamo Oktoba. 2016 anapodai kuwa amehitimu.