“Hakuna kitu hushusha ulevi kama kofi katika shavu la pili,” Moses Kuria amwambia rais Kenyatta

Katika mkutano wa viongozi wa kidini kutoka mlima Kenya, rais Kenyatta alisema angepigwa kofi angegeuza shavu la pili pia apigwe.

Muhtasari

• Moses Kuria ambaye anamtetea vikali Ruto dhidi ya masimango ya Uhuru Kenyatta anazidi kumshambulia rais bila kutetereka.

Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria na rais Uhuru Kenyatta
Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria na rais Uhuru Kenyatta
Image: Moses Kuria, State House Kenya (Facebook)

Mbunge wa Gatundu ya Kusini Moses Kuria anaonekana hayuko karibu na kusitisha maneno yake makali ya kumshambulia rais Uhuru Kenyatta.

Mbunge huyo ambaye ni wa nyumbani kwake Uhuru Kenyatta amekuwa kwa muda sasa akimshambulia vikali rais tena kwa kutumia maneno ya nguoni yasiyokuwa na heshima hata kidogo kwa rais aliye mamlakani.

Kuria ambaye analenga kuwa gavana wa kaunti pana ya Kiambu kupitia tikiti ya chama chake cha Kazi, ni mwandani mkubwa wa naibu rais William Ruto, na inavyoonekana amejukua jukumu la kujitwika suala zima la ugomvi wa rais na naibu wake ambapo amevivaa viatu vya Ruto na kuwa na mwendelezo wa kumshambulia Kenyatta kwa niaba yake.

Suala la Ruto kutaka kumzaba Kenyatta kwa kofi kali baada ya Kenyatta kudaiwa kutaka kususia kushiriki uchaguzi wa marudio wa 2017 limekuwa gumzo kubwa kwa wiki sasa baada ya mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed kuvujisha sauti ya Ruto akisema hivyo.

Jana wakati wa kikao na viongozi wa kidini kutoka eneo pana la Mlima Kenya katika ikulu ya Nairobi, rais Uhuru Kenyatta kwa mara ya kwanza alizungumzia suala hilo na kukubali kwamba alikuwa na nia ya kuacha kuwania urais katika uchaguzi huo wa marudio ambao jaji mkuu David Maraga aliharamisha uchaguzi wa awali kwa madai ya wizi na udanganyifu.

Raia Kenyatta alijitetea mbele ya viongozi wa kidini akisema kwamba lengo lake kutaka kususia lilikuwa ni kuhepusha vita na umwagikaji wa damu katika uchaguzi huo uliozua nyufa kubwa baina ya wananchi.

Kenyatta alisema kwamba kama kweli Ruto alikuwa na nia ya kumzaba, basi angemgeuzia na upande wa shavu lingine na kumuamuru kumzaba pia kama ambavyo biblia inavyoagiza. Kenyatta alikuwa akizungumza haya kwa lugha yake ya Mama – Kikuyu.

Sasa mbunge wa nyumbani kwake Moses Kuria ameibua madai kwamba yeye kusema angekubali kuzabwa kofi shavu lingine si vibaya kwani kofi katika shavu ni moja ya tiba kubwa za kuondoa ulevi kichwani kwa haraka mno.

“Hakuna kitu hushusha ulevi kama kofi katika shavu la pili,” Kuria aliandika, akionekana kushambulia na kukejeli maneno ya rais kwamba angekubali kuzabwa shavu la pili.