Ruto: Raila ameanguka mara tano, angekuwa nguo angeitwa mtumba

Ruto alisema Raila hafqai kusema mitumba ni nguo za wafu kwani hata yeye angekuwa nguo angeitwa mtumba.

Muhtasari

• “Kwani kuvaa mitumba ni dhambi? Kwani kuvaa mitumba ni hatia? Na tumewaambia punguzeni madharau kidogo na mkizidi tutakutana kwa debe" - Ruto

Kinara wa ODM Raila Odinga na Kinara wa UDA William Ruto
Kinara wa ODM Raila Odinga na Kinara wa UDA William Ruto
Image: Maktaba

Mpeperusha bendera wa vuguvugu la Kenya Kwanza katika kinyang’anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Dkt. William Ruto amemlinganisha mpinzani wake mkuu Raila Odinga na nguo za Mitumba kwa kile alisema kwamba Odinga amejaribu bahati yake mara nyingi katika nafasi ya urais na kudunda na hivyo angekuwa nguo basi ni ile ya mtumba.

Akihutubia umati kwenye kaunti ya Taita Taveta katika moja ya kampeni za kunadi sera zake kwa wananchi, Ruto alimsuta vikali Raila Odinga kwa kusema kwamab nguo za mitumba ni za watu waliokufa na kusema kwamba hata yeye ni mtumba kwa sababu amejaribu siasa mara nyingi na kufeli safari zote nne alizowania kama rais.

“Kwani kuvaa mitumba ni dhambi? Kwani kuvaa mitumba ni hatia? Na tumewaambia punguzeni madharau kidogo na mkizidi tutakutana kwa debe. Sasa huyu bwana Kitendawili anapigana mitumba, hataki mitumba. Niwaulize, kama angekuwa nguo, ameanguka mara tano, kama alikuwa nguo si yeye tayari angekuwa mtumba. Sasa mtumba moja inashindana na mtumba ingine?” Ruto alisema huku umati ukimshangilia.

Vile vile Ruto alimshambulia Raila kwa kusema kwamba hana sera kando na ile misemo yake kwa vijana ambayo naibu huyo wa rais alisema ni kama hekaya za abunuwasi kwani haiwezi kuwapa vijana ajira.

“Tafadhali tuambizane mambo ya ukweli. Hawa vijana tukiwaambia tibim tialala ndio watapata ajira? Si huo ni upuzi? Si huo ni upumbavu? Hekaya za abunuwasi tialala tibim ya upuzi?” William Ruto alitupa bomu la moto kwa kambi ya Raila.

Kinara huyo wa Kenya Kwanza aliwarai wakaazi wa eneo hilo la pwani kumpigia kura kama rais wa tano kwa kuwa bado kuna deni lao alilowaahidi katika kampeni za awali za 2017 kuhusu kuwawekea miradi mbali mbali eneo hilo.

Viongozi hao wawili wanazidi kumenyana katika kampeni huku zikiwa zimesalia chini ya wiki tatu tu kuelekea debeni.

Ruto na Raila wanatarajiwa kumenyana wiki kesho katika mdahalo mkali wa urais unaosubiriwa na Wakenya wengi.