Msimu wa uchaguzi umetimia huku wanasiasa wakizidi kuhadaa wakenya

Kwa miaka mingi wakenya wamekuwa wakipiga kura kwa misingi ya kikabila na ahadi za uongo

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta ameacha msingi thabiti wa kuendeleza miradi ya  maendeleo nchini.

Umati wa wananchi wakihudhuria mkutano wa hadhara
Umati wa wananchi wakihudhuria mkutano wa hadhara
Image: AZIMIO TV

Kwa miaka mingi wakenya wamekuwa wakipiga kura kwa misingi ya kikabila na  ahadi za uongo. katika kinyang'anyiro cha Agosti 9 ni vyema kuepuka tofauti hii na kuzingatia  sera  na wala si ukabila tena.

Vita vimeshuhudiwa na mikwaruzano kila kura inapopigwa,  mwaka wa 2007 wakenya wengi walipoteza maisha yao kutokana na mauaji baina ya makabila. Wengi walipoteza kazi, makazi na kilichokuwa cha thamani kubwa kwao. Mwaka wa 2017 kulishuhudiwa  migomo,vifo na kesi ya kupinga matokeo ya urais katika mahakama ya upeo ambayo hakika ilifanya kila jitihada kutoa hukumu vilivyo. Uhasama wa kisiasa ulitulizwa tulizwa tu baada ya "handshake".

Je, ni wakenya hawaaminiki au ni tatizo la maafisa wa tume huru ya mipaka na uchaguzi (IEBC)? Ikiwa ni upigaji kura wakenya wanawajibika vilivyo  lakini ifikaapo kwenye kuhesabu, takwimu  zinatupiga chenga. Twaomba hali hii isitokee tena katika uchaguzi mkuu mnamo Agosti, ni vyema kwa IEBC kuwajibika ipasavyo.

Wagombea kiti cha urais na nyadhifa zingine, watupilie mbali dhana ya ukabila usiokuwa na misingi yeyote na kupigia upato sera jenzi kwa faida ya mwananchi wa kawaida.Elimu, Afya bora,kilimo na biashara,maji,kazi kwa vijana iwe baadhi ya maswala  ambayo mgombea atatakiwa kudadavua na kueleza  mikakati ya kuyafanikisha. Hatutataki ahadi za uongo tena.

Mabilioni ya pesa yanatumika katika kampeni  za kutafuta uungwaji mkono huku wananchi wanaoishi katika hali ya uchochole wakipumbazwa tu kwa shilingi hamsini, kuuza kura zao kwa hawa nguli wasiojua umuhimu na swala zima la uongozi. Mbona haya mabilioni hayatumiki kuboresha uchumi na hali ya maisha ya wakenya?.

Rais Uhuru Kenyatta ameacha msingi thabiti wa kuendeleza miradi ya  maendeleo nchini, licha ya kwamba baadhi ya wananchi wanahisi ya kwamba miradi mingine haiwafaidi moja kwa moja,  kuna uwezekano huu ukawa mwanzo wa sura mpya kwa sababu ameng’amua umuhimu wa huduma Kwa wakenya.Hospitali ngapi zimejengwa?barabara ngapi  zimeimarishwa kuwafaidi wawekezaji katika sekta za usafiri na kilimo?

Chini ya himaya yake hata hivyo amewahifadhi "wakuu" wa sakata ambao wamekuwa  tandabelua katika ujenzi wa taifa, Kinachonifurahisha  ni kwamba limbukizi wanajulikana. Waliohusishwa na sakata yoyote ile wasiteuliwe katika kinyang'anyiro hicho,wacha liwe funzo kwa wengine.

Mwisho, amani ya wakenya ni muhimu sana kuliko kampeni za kutaka kura, wapiga kura wasiruhusu kulaghaiwa na wanasiasa wenye fikra potovu,wasimame kidete kuwachagua viongozi wenye maono na ari ya kutekeleza sera zao.