Ruto Adokeza Kufanya 'Handshake' na Raila Baada ya Uchaguzi "Niko Tayari kunywa Chai na Yeye"

DP Ruto alisisitiza kwamba licha ya kunywa chai lakini bado hatachanganya serikali na upinzani.

Muhtasari

• Ruto alizidi kusisitiza kwamab chai ya pamoja watakunywa kwa sababu wao wote ni wakenya na pia ni ndugu.

Kinara wa ODM Raila Odinga akisalimiana na naibu rais William Ruto
Kinara wa ODM Raila Odinga akisalimiana na naibu rais William Ruto
Image: Maktaba

Mpeperusha bendera wa muungano wa Kenya Kwanza, William Ruto kwa mara nyingine tena amedokeza uwezekano wa kuwa na ‘handshake’ na mpinzani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha urais kutoka Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga baada ya kukamilika kwa heka heka za uchaguzi mkuu Jumanne Agosti 9.

Akizungumza katika uwanja wa Nyayo katika kongamano la kuhitimisha kampeni kulingana na makataa ya katiba, Ruto aisema kwamba yeye ako tayari baada ya kushinda uchaguzi huo na kuapishwa, atamuita Raila Odinga ili wakunywe chai pamoja na kuzika tofauti zao za kisiasa.

“Mimi nimemuambia rafiki yangu bwana Kitendawili (Raila Odinga) ya kwamba mimi niko tayari kunywa na yeye chai baada ya Jumanne. Lakini yale mambo ambayo sitafanay ni yale yalifanyika miaka mitano iliyopita, mambo ya kuchanganya upinzani na serikali na kutengeneza kitu ambacho Wakenya hawakijui, ya kuhujumu katiba ya Kenya, ya kuleta uhasama na vurugu, hayo mimi sitafanya!” Ruto alizungumza huku umati mkubwa kama siafu uliofurika Nyayo ukimshangilia kwa vifijo.

Ruto alizidi kusisitiza kwamab chai ya pamoja watakunywa kwa sababu wao wote ni wakenya na pia ni ndugu.

Kauli hizi za Ruto zinawiana na kauli za baadhi ya wachanganuzi wa kisiasa ambao wamekuwa wakikisia kwamba baada ya uchaguzi mkuu haijalishi nani ataibuka mshindi kati ya Ruto na Raila, wawili hao kuna mmoja atamtafuta mwingine kwa ajili ya kutafuta suluhu ya amani almaarufu Handshake na hivyo kumtenga rais Kenyatta ambaye kwa sasa ameonesha tofauti zake na naibu wake hadharani huku akimpendelea aliyekuwa mshindani wake katika uchaguzi uliopita, Raila Odinga.

Rais Kenyatta baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa 2017 uliokuwa na ushindani wa aina yake kati yake na Raila Odinga, alimtafuta Odinga kisiri na kukubaliana kuzika tofauti zao kweney kaburi la sahamu na kuanza kufanay kazi pamoja mnamo mwezi Februari mwaka 2018, jambo ambalo lilimkera naibu rais William Ruto aliyejiweka pembeni kutoka harakati za serikali ya Jubilee na kumuachia rais Kenyatta akifanya mambo mengi kwa kushirikiana na Odinga.