IEBC yaidhinisha matumizi ya sajili mbadala baada ya KIEMS kufeli

Hatua hii imetokana na hitilafu katika baadhi ya mitambo ya KIEMS kit ambayo ilikuwa itumike.

Muhtasari

• Tume ya uchaguzi pia imeelezea kulemazwa kwa shughuli za uchaguzi katika eneo la Eldas kutokana na utovu wa usalama.

Naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera
Naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera

Tume ya uchaguzi na mipaka IEBC imelazimika kuidhinisha matumizi ya sajili iliyochapishwa ya wapiga kura katika baadhi ya maeneo.

Hatua hii imetokana na hitilafu katika baadhi ya mitambo ya KIEMS kit ambayo ilikuwa itumike.

Naibu mwenyekiti wa tume ya IEBC Juliana Cherera alisema kwamba maeneo ambayo wameidhinishwa kutumia sajili zilizochapishwa ni katika kaunti ya Makueni eneo la Kibwezi West na Kakamega maeneo ya Malaba, Matungu, Mumias West na Mumias East.

IEBC Hata hivyo imewahakikishia wananchi kuwa ni idadi ndogo sana ya vifaa vya KIEMS kits vilivyokuwa na hitilafu.

Tume ya uchaguzi pia imeelezea kulemazwa kwa shughuli za uchaguzi katika eneo la Eldas kutokana na utovu wa usalama.  Tume imesema kwamba kuna makabiliano makali baina ya vikosi vya usalama na wavamizi.

Maafisa wa uchaguzi wamelazimika kutafuta hifadhi wakihofia maisha yao, huku milio ya risasi ikirindima eneo hilo.

IEBC hata hivyo imeahidi kuendelea na uchaguzi punde tu hali ya utulivu itarejea au kuahirisha uchaguzi huo hadi kesho.

Cherera alisema kwamba utovu wa usalama umeathiri kuanza kwa shughuli ya uchaguzi katika eneo la Dadaab huku baadhi ya vituo vikikosa kufunguliwa.

Huku hayo yakijiri maafisa watatu wa tume ya IEBC waliokuwa safarini kusimamia uchaguzi katika kaunti ya Turkana wamelazwa katika hospitali baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani. Wawili walikuwa makarani na mmoja afisa mkuu wa uchaguzi. Tume imesema tayari imetuma maafisa wengine kuendesha shughuli hiyo.

Tume imewakakikishia wananchi kuwa muda wote ambao umepotea kutokana na kucheleweshwa kufunguliwa kwa kituo cha uchaguzi utafidiwa.

Kulingana na kanuni za uchaguzi zoezi la upigaji kura linafaa kuanza saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni.