Jina la Ngilu laonekana kwenye karatasi za kupiga kura licha ya kujitoa awali

Ngilu alikuwa analenga kuwania kama gavana kwa muhula wa pili

Muhtasari

• Katika baadhi ya picha za karatasi za kupiga kura hizo ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, jina la Ngilu linaonekana kwenye karatasi za ugavana

PAMOJA gavana wa Kitui Charity Ngilu na mwaniaji ugavana David Musila katika hafla ya awali katika mji wa Kitui.
PAMOJA gavana wa Kitui Charity Ngilu na mwaniaji ugavana David Musila katika hafla ya awali katika mji wa Kitui.
Image: Maktaba

Sintofahamu ilikumba macho ya wapiga kura kaunti ya Kitui baada ya jina la gavana wa sasa Charity Ngilu kuonekana kwenye karatasi za kupiga kura licha ya gavana huyo kuweka wazi wiki kadhaa zilizopita kwamba amejitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Katika baadhi ya picha za karatasi za kupiga kura hizo ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, jina la Ngilu linaonekana kwenye karatasi za ugavana za kupiga kura likiwa la mwisho pamoja na mgombea mwenza wake Gideon Nzau, huku waliokuwa wakimenyana naye kwenye kipute cha ugavana Kitui wakiwa ni gavana wa kwanza Julius Malombe ambaye aliwania na Wiper, Jonathan Mueke wa UDA na David Musila wa Jubilee.

Takriban mwezi mmoja uliopita, wakati wa kampeni za muungano pana wa Azimio la Umoja One Kenya, kinara wao Raila Odinga alitangaza kwamba angempa Ngilu kazi katika serikali kuu na kutangaza kwamba Kitui wangemuunga mkono gavana wa zamani Julius Malombe.

Inaarifiwa baadae Ngilu aliwataarifu wakaaji wa Kitui kutompigia kura kwani sasa ashaweka pembeni azma yake ya ya kuwania kipindi cha pili kama gavana na badala yake kuwataka wampigie kura malombe.

Inaarifiwa IEBC ilisema kwamba kipindi cha kutangaza kujitoa kwake katika kinyang’anyiro cha ugavana, tayari karatasi za kupiga kura zilikuwa zimepigwa chapa na majina ya wagombea wote ugavana wakiwa wamewekwa pamoja na nembo za vyama vyao.