Patanisho: Mwanadada agura ndoa ya miaka 10 baada ya mumewe kuhusika kwenye ajali na kupoteza kazi

Muhtasari

•Evans alisema ndoa yake ya miaka kumi ilisambaratika mwezi baada yake kuhusika kwenye ajali na kupoteza kazi yake mwezi Januari mwaka huu.

•Evans alikiri kwamba kabla ya mke wake kuondoka walikuwa wamevurugana na kutupiana maneno makali.

•Eunice alipopigiwa simu alikiri kuwa anamfahamu Evans vizuri ila akasita kuzungumza naye wasuluhishe mzozo wao.

Gidi na Ghost asubuhi
Gidi na Ghost asubuhi

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Evans Obara (28) kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke  wake Eunice (28) ambaye  walikosana mapema mwaka huu.

Evans alisema ndoa yake ya miaka kumi ilisambaratika mwezi baada yake kuhusika kwenye ajali na kupoteza kazi yake mwezi Januari mwaka huu.

Alisema mke wake aliondoka pamoja na watoto wao wawili akilalamikia hali ya mumewe kukosa kazi.

"Nilipata ajali 2019 mwezi wa nane nikawa nimevunjika mkono. Nilipoenda hospitali niliambiwa nipumzike mwaka moja. Kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja nilirudi nyumbani mapato ikawa chini kidogo. Kufuatia hayo akapiga simu nyumbani kwao akasema eti nahatarisha maisha yake. Ndugu yake akachukua hatua hata bila kuniarifu akamtumia nauli akaenda kwao na watoto" Evans alisema.

Evans alikiri kwamba kabla ya mke wake kuondoka walikuwa wamevurugana na kutupiana maneno makali.

Alisema tayari amepiga hatua kadhaa za kujaribu kumrejesha mke wake nyumbani ila juhudi zake hazijazaa matunda kufikia sasa.

"Nimejaribu sana kujaribu kupatana familia kwa familia lakini naona kama ndugu zake ndio wamemkalia asirudi. Nimejaribu mambo mingi, nimemtumia wazazi, wajomba, ndugu zangu na hata marafiki zake. Leo niko patanisho, natafuta tu mashahidi kwa wingi kwa sababu najua kuna wakati watoto watakuja kuuliza swali. Nimejaribu imeshindikana ni sawa tu" Evans alisema.

Eunice alipopigiwa simu alikiri kuwa anamfahamu Evans vizuri ila akasita kuzungumza naye wasuluhishe mzozo wao.

Evans alipopatiwa nafasi ya kuomba msamaha Eunice alikata simu mara moja na kuizima kuashiria kuwa hakutaka kunena na baba ya watoto wake.

Evans alikubali hali ilivyokuwa ila akaomba mkewe asije akamrudishia watoto baada ya kushindwa kuwalea kwani alitaka washirikiane katika ulezi.