Patanisho: Fundi wa stima aachwa baada ya kuchukuliwa na mwanamke mwingine na kulala nje siku tatu

Muhtasari

•Mary alifichua kwamba mwanamke huyo amekuwa akimchukua mumewe kwa gari lake mara kwa mara na kuenda naye kwa kipindi cha  hadi wiki moja

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Obara alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Mary  ambaye alidai alimuacha baada yake kuenda kazi nje kwa kipindi cha siku tatu.

Obara alisema kuna mwanamke fulani ambaye alimpatia kazi ya kutengeneza stima iliyofaa kuchukua siku moja ila kutokana na ukosefu wa fundi wengine akaifanya pekee yake kwa siku tatu bila kuenda nyumbani.

Alieleza  hakumfahamisha mkewe kuwa angelala nje siku tatu kwa kuwa alihofia kwamba hangekubali kumuelewa. Alisema aliporudi nyumbani alipata mkewe akiwa amefura kama kaimati na baada ya kujibizana kwa muda porudi akatoka akaenda na kumuachia watoto.

"Mimi ni fundi wa kuunganisha stima. Kuna mama alikuja akaniitia kazi ya kuunganisha stima kwa nyumba yake iliyo mjini Kisii. Ilikuwa kazi ya siku moja unusu hivi lakini kwa sababu wenye walikuwa wanisaidie hawakuingia ikabidi sasa nifanye kazi mara dufu na nikaifanya siku tatu. Mke wangu ni mkaidi, niliona hata nikipiga simu hatutaelewana. Nilifanya kazi nikalipwa,kurudi nyumbani nikapata amenuna kweli kweli. Alianza kuniuliza maswali hata kabla sijaweka vyombo chini. Baadae akafunga virago nikiangalia akaniachia watoto akaenda" Obara alisimulia.

Obara alieleza kwamba mwanamke aliyekuwa amempatia kazi alimchukua nyumbani kwake kwa gari lake akampeleka kwa nyumba ya wageni ambayo anamiliki. Hata hivyo alifichua kwamba mwanamke huyo ameolewa na hakukuwa na mipango mingine fiche kati yao.

"Sina mipango ya kando. Mimi hufanya kazi hivo tu" Obara alijitetea.

Mary alipopigiwa simu alifichua mengi kuhusu uhusiano wa mumewe na mwanamke ambaye alidai alikuwa amempatia kazi ya kutengeneza stima.

Alifichua kwamba mwanamke huyo amekuwa akimchukua mumewe kwa gari lake mara kwa mara na kuenda naye kwa kipindi cha  hadi wiki moja. Mary alisema jambo lile lilikuwa limemchosha na ndio maana alifanya maamuzi ya kuondoka.

"Huyo mwanamume amekuwa akinisumbua na huyo mwanamke ambaye amekuwa akimchukua  na gari. Anakuja hadi kwa nyumba anamchukua na ni mama wa miaka 55. Anamchukua eti wanaenda kutengeneza stima. Nashangaa anatengeneza stima siku tatu, mara siku mbili, siku nne nikachoka kwa kuwa nilikuwa nalala pekee yangu kwa kitanda. Wanaenda hata wiki moja" Mary alifichua.

Obara alijaribu kumweleza mkewe kwamba mwanamke yule ni mmoja wa wateja wake wengi. Alisema kuwa mwanamke yule anamiliki nyumba nyingi na ndiposa huwa anampatia kazi mara kwa mara.

Obara alimsihi Mary aelewe kazi mahitaji ya kazi yake huku akimuomba arejee nyumbani waendelee kulea watoto wao wachanga.

Mary alikubali kumsamehe mumewe na kumhakikishi kwamba angerudi nyumbani hivi karibuni iwapo angemtumia nauli.