Rev. Serunjogi - Mwanaume anayesaliti mkewe hupoteza furaha, kwama na mkeo!

Mchungaji huyo alisema pete ya ndoa si kitu cha kufanyiwa mzaha.

Muhtasari

• Kila wakati unapofanya mapatano, hakikisha unatimiza wajibu wake - Serunjogi

Mchungaji anasema wanaume wanaosaliti wake zao hupoteza furaha
ESMOND SERUNJOGI Mchungaji anasema wanaume wanaosaliti wake zao hupoteza furaha
Image: FACEBOOK//SCREENGRAB

Mchungaji mmoja kwa jina Esmond Serunjogi amewataka watu waliokula Yamini ya kuingia katika ndoa takatifu na kuvalisha pete kutolifanyia suala hilo mzaha kwani ni jambo ambalo Mungu analichukulia kwa njia ya kitakatifu mno isiyofaa kufanyiwa mchezo.

Akizungumza katika kituo kimoja cha runinga, Serunjogi aliwataka wanaume walioingia katika ndoa takatifu kukoma kuchepuka kwa wake zao kwani kutoka nje ya ndoa ndio mwanzo wa kupoteza furaha yako na Kwenda mbele utakuwa unaigiza furaha tu ila kutoka moyoni hautakuwa na furaha wala amani.

“Kuweka pete kwa mtu pia ni ishara ya chaguo. Ina maana kwamba mpenzi wako amekuchagua kutoka kwa wengine. Usivae pete yenye maana ambayo huna uhakika nayo. Pete inaweza kubeba baraka au laana. Watu hulia juu ya pete zao. Wengine hufanya ibada na mengi zaidi,” alinukuliwa mchungaji Serunjogi.

Mchungaji huyo pia alizidi kufafanua zaidi maana na nguvu za pete ya ndoa takatifu huku akisema kwamba nguvu zake ni za kipekee na ndio maana watu wengine hata baada ya kuzurura mbali na ndoa zao bado hujipata wamerudi tu katika ndoa zao kutokana na nguvu za pete ya ndoa.

“Pia tunazingatia pete ya ndoa kama ushuhuda wa upendo usio na kikomo na usio na masharti. Ndio maana wenzi wengine huwa wanapata njia ya kurudi kwenye ndoa zao halali hata baada ya kuzurura. Pete ni ishara ya kujitolea kwa mwenzi wako. Kamwe, kwa wakati mmoja, usifikirie kuwa ndoa halali ni kama uhusiano mwingine wowote. Mtu anayeweka pete kwenye kidole chako ana haki ya kukudai,” Serunjogi alitoa ufunuo wenye tija kuhusu pete ya ndoa.

Kulingana na mchingaji Serunjogi, kumvalisha mtu pete ya ndoa ni kama kula kiapo cha kutomsaliti na endapo utamsaliti kwa kuchepuka nje ya ndoa basi huo ndio mwisho wa kutengana wewe na furaha yako.

“Kumvisha mtu pete maana yake ni kufanya agano. Hakuna mwanamume aliyeoa ambaye anapata furaha baada ya kusaliti mke wake. Naam, wanaume hao hujifanya kuwa na furaha lakini ukweli ni kwamba hawana furaha. Kila wakati unapofanya mapatano, hakikisha unatimiza wajibu wake. Kuna matokeo ya mapatano hayo, mazuri na mabaya. Ndio maana watu wasiokatisha ndoa za zamani hawapati amani baada ya kujiunga na mahusiano mapya,” mchungaji Serunjogi.