Bruce Melodie wa Rwanda awapatanisha Bahati na Harmonize kuzika bifu

Mwaka 2020 Bahati aliwahi kumshambulia vikali Harmonize kwa kuanzisha uadui na Diamond Platnumz.

Muhtasari

• Bifu la Harmonize na Bahati lilianza mapema mwaka 2020 baada ya msanii huyo kutoka Kenya kuanza kumshambulia Harmonize akimtaka kutafuta suluhu la Amani na Diamond.

Bahati na Harmonize wakipatanishwa na Bruce Melodie
Bahati na Harmonize wakipatanishwa na Bruce Melodie
Image: Instagram//Brice Melodie

Msanii wa kizazi kipya nchini Kenya Kevin Bahati hatimaye amemaliza uhasama wake na staa kutoka Tanzania, Harmonize.

Japo wawili hao hawajazungumza wazi kuhusu hilo, lakini ilidhihirika baada ya msanii kutoka Rwanda Bruce Melodie kupakia picha akiwa kama anawapatanisha wawili hao.

Walikuwa wamekutana katika tamasha la msanii wa Uganda Eddy Kenzo ambapo Melodie alionekana kuwa katikati yao huku wakisalimiana kwa tabasamu.

Bifu la Harmonize na Bahati lilianza mapema mwaka 2020 baada ya msanii huyo kutoka Kenya kuanza kumshambulia Harmonize akimtaka kutafuta suluhu la Amani na Diamond – kipindi hicho ndio Harmonize alikuwa ameondoka WCB ya Diamond kwa shari ya aina yake.

Bahati aliendelea kumshambulia Harmonize akimwambia kwamba alikuwa anajaribu kulazimisha bifu na Harmonize na kumtemea moto usoni kuwa katu hawezi kumfikia mkurugenzi huyo wa WCB kimuziki.

Kipindi hicho, Harmonize alionekana kukaa kimya kabisa lakini alizungumza kwa vitendo ambapo alifuatisha kwa kum-unfollow Bahati kwenye mtandao wa Instagram.

Bahati alikitaja kitendo hicho kama cha kike na kumtaka Harmonize amzungumzie moja kwa moja kwa alikuwa anamshauri jambo la maana kuacha kupalilia uhasama na Diamond.

“Unajua hautarajii ukimwambia rafiki yako ukweli, achukuliwe kwa ndani mpaka anaku unfollow hayo ni mambo ya kike. Ninaheshimu sana talanta ya Harmonize lakini pia ninaheshimu tamaduni zetu za Kiafrika kwamba anaweza akaenda mbali zaidi akifanya Amani na mtu yeyote ambaye alimshika mkono kuinuka,” Bahati alisema kipindi hicho kwenye mahojiano fulani na blogu moja.

Baada ya Melodie kupakia picha hiyo akiwa kama anawasikiliza wawili hao wakinong’onezeana huku wameshikana mikono, wengi walihisi huenda ndio mwanzo wameafikiana kuzika tofauti zao na kufanya kazi pamoja kama wanamuziki wa Afrika Mashariki.