Diamond amtetea Alikiba dhidi ya kauli za watu kuwa Crown Media si yake

Baadhi ya watu walijitokeza na kauli kwamba Crown Media si ya Alikiba bali ni ya wakwasi Fulani ambao wamemtumia Alikiba kama njia moja ya kupata ufanisi.

Muhtasari

• Diamond pia alisema kwamba ni wakati wasanii wote wenye uwezo waendelee kufanya mambo makubwa ili kuondoa kile kilichokuwa kikisemwa kwamba usanii ni uhuni.

Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amemtetea mshindani wake wa muda mrefu, Alikiba dhidi ya kauli za watu kuhusu umiliki wa chombo cha habari, Crown Media.

Alikiba alitangaza kuzinduliwa kwa Crown Media takribani mwezi mmoja uliopita lakini tangu hapo bado kituo cha redio na runinga havijaanza kupeperusha matangazo yao hewani moja kwa moja.

Baadhi ya watu walijitokeza na kauli kwamba Crown Media si ya Alikiba bali ni ya wakwasi Fulani ambao wamemtumia Alikiba kama njia moja ya kupata ufanisi.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani siku mbili zilizopita, Diamond ambaye pia ni mmiliki wa chombo cha habari – Wasafi Media – alimtetea Alikiba akisema kwamba ni hatua nzuri aliyopiga kujikita katika uwekezaji wa kwenye vyombo vya habari.

Diamond pia alisema kwamba ni wakati wasanii wote wenye uwezo waendelee kufanya mambo makubwa ili kuondoa kile kilichokuwa kikisemwa kwamba usanii ni uhuni.

Diamond pia alikanusha madai ya watu kwamba Alikiba alianzisha media yake kama njia ya kuzidisha ushindani dhidi yake, akisema kwamba ni njia nzuri na yeyote mwenye uwezo pia afungue ndio zikuwe nyingi.

“Siwezi kusema kwamba Alikiba alifungua media eti kwa sababu pia mimi nina media, hii ni hatua kubwa sana kwetu wasanii, nafikiri hilo ni jambo zuri kwake. Tena nimeona kuna wale wanaosema hii media sio ya Alikiba mwenyewe, sio tatizo ndio mana zikaitwa media company,” Diamond alisema.

Siku chache zilizopita wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Alikiba aliulizwa kwa nini bado vipindi havijaanza kupeperushwa moja kwa moja hewani, alisema kwamba mipango ilikuwa inaendelea na kuahidi kwamba media hiyo ingeteka anga zote pindi Ramadhani itakapokamilika.