Sonko alalama kuzuiliwa kutoa msaada kwa mtoto Sagini, asema siasa imeingizwa

Sonko alisema mtoto huyo alitarajiwa kukutana na daktari wa macho Nairobi lakini hilo halijafanyika kwa mara tatu sasa.

Muhtasari

• Alisema kuwa watu fulani wameanza kumzuia wakidhani ni PR anafanya kwa suala la afya ya mtoto Sagini.

• Mtoto Sagini alinyofolewa macho wiki mbili zilizopita na watu wasiojulikana.

Mike Sonko alalama kunyimwa kutoka msaada kwa mtoto Sagini
Mike Sonko alalama kunyimwa kutoka msaada kwa mtoto Sagini
Image: Facebook

Mhisani mwema na ambaye alikuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amelalamika vikali kuhusu njama ya baadhi ya watu kutoka kaunti ya Kisii ambao wanajaribu kumzuia kutotoa msaada kwa mtoto Sagini aliyenyofolewa macho na watu wasiojulikana.

Kupitia video moja ambayo Sonko alikuwa anazungumza na watu kupitia ukurasa wake wa Facebook, alisema kuwa suala la afya ya mtoto Sagini limechukuliwa kisiasa na baadhi ya watu kutoka Kisii ambao sasa wameanza kupiga vita hatua yake ya kutoa msaada kwa kumtafutia mtoto huyo daktari wa macho ili kujaribu kuona kama kuna uwezekano wa kupata kuona tena baada ya kupoteza macho.

“Pamoja na jitihada zangu za kuwasaidia sijaweza kuzifanikisha kutokana na siasa mbovu zinazochezwa na baadhi ya wanasiasa wenye fikra chafu wanaodhani niko katika kesi hii kwa malengo ya PR na kisiasa lakini hilo halitanizuia kuendelea na suala hilo. Ninatuma zawadi zao ndogo za Krismasi kupitia kwa msamaria mwema ambaye pia anasaidia uwanjani kwa familia ya Esnahs Nyaramba,” Sonko alisema.

Sonko alisisitiza kuwa yeye hana haja yoyote ya kuwania wadhifa wa kisiasa katika kaunti hiyo na kuonesha kusikitishwa kwake na hatua ya baadhi ya watu kuzuia msaada wake huku akisisitiza kuwa yeye hajawahi tafuta kiki kwa kutoa msaada.

Pia alisema patashika hiyo imesababisha mtoto Sagini kukosa kukutanishwa na daktari mmoja wa macho eneo la Westlands Nairobi kutokana na kuzuiwa kumfikia kwa msaada huo.

“Wiki iliyopita Baby Sagini alikosa miadi mara mbili muhimu na Dk. Kishor katika hospitali ya macho ya laser ya Westlands sababu tulitaka ripoti ya mapitio ya mtoto itumwe kwa barua pepe China ili tuanze mchakato wa kumpeleka huko kwa ajili ya kupandikizwa macho ya bandia. Kulitia siasa suala hilo na kuninyima kumfikia yeye na dada yake hakutanizuia kusaidia,” Sonko alilalama.

“Kwa kawaida sifanyi PR ninaposaidia watu. Nimefanya kwa mafanikio mara nyingi. Kwa hiyo tuwache siasa mbaya mimi sitaki kiti yoyote Kisii na hakuna kampeni zinaendelea kwa sasa.”