"Aki Nairobi! Ahsante sana," Sakaja baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi

Sakaja alimbwaga Igathe wa Jubilee katika kipute hicho

Muhtasari

• "Nawapenda sana na niko tayari kuwatumikia,” aliandika Sakaja kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Gavana mteule wa Nairobi Johnson Sakaja pamoja na naibu wake wakiwa wameshika cheti cha ushindi
Gavana mteule wa Nairobi Johnson Sakaja pamoja na naibu wake wakiwa wameshika cheti cha ushindi
Image: JOHNSON SAKAJA//FACEBOOK

Gavana mteule wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amewashukuru sana wakaazi wa Nairobi waliomchagua na kuwataka sasa kujiunga na yeye katika safari ya kuirudisha kauti hiyo inayotajwa kuwa kitovu cha Kenya katika ubora wake.

Baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi asubuhi ya Jumapili katika ukumbi wa Kasarani na msimamizi mkuu wa usimamizi wa kaunti hiyo Albert Gogo, Sakaja alienda nje kusherehekea katika kucheza densi nzuri na mashabiki wake waliofurika nje baada ya kutoruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo.

Sakaja aliwahakikishia wana Nairobi wote hata wale hawakumchagua kwamba atawadhibitishia machoni mwao vinginevyo kwa kuwafanyia kazi pasi na mwegemeo au ubaguzi wowote.

“Aki Nairobi! ASANTENI SANA! Sasa tembea nami safari hii ili tuweke utaratibu wa jiji letu, tuwape watu wetu utu, tutoe matumaini na fursa kwa wote. Nawapenda sana na niko tayari kuwatumikia,” aliandika Sakaja kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Sakaja alitangazwa mshindi baada ya kujinyakulia kura zaidi ya laki sita na mia tisa huku mshindani wake wa karibu Polycarp Igathe kutoka chama cha Jubilee akiibuka wa pili na kura zaidi ya laki tano.

Sakaja alikuwa akiwania kupitia tikiti ya chama cha naibu rais William Ruto, UDA.