Edwin Sifuna Ashinda Useneta Nairobi

Sifuna Sasa atachukua wadhifa huo kutoka kwa seneta wa Nairobi Johnson Sakaja

Muhtasari

• Askofu Margaret Wanjiru kutoka UDA alipata kura 554, 091.

Mgombea useneta wa Nairobi kwa tiketi ya ODM Edwin Sifuna
Image: TWITTER// EDWIN SIFUNA

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ameshinda kiti cha Seneta wa Nairobi baada ya kupata kura 716,876. Askofu Margaret Wanjiru kutoka UDA alipata kura 554, 091.

Sifuna Sasa atachukua wadhifa huo kutoka kwa seneta wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye anawania kiti cha ugavana wa jiji hilo.

Wengine waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni Silas Angira (Chama cha Democratic Unity), David Mwangi Gichuru (Safina), Abdikadir Ahmed Jamaa (Usawa kwa Wote Party), William Wahome Kabera (Democratic Party of Kenya), Julie Wanjiru Kabogo (Chama Cha Kazi), na Jacintah Wambui Kamau (Chama cha Kikomunisti cha Kenya).

Msimamizi wa Uchaguzi wa Kaunti ya Nairobi Albert Gogo Nguma alimpa Sifuna cheti huku kukiwa na shangwe katika ukumbi huo wa Kasarani ambako ndicho kilikuwa kituo kikuu cha kuhesabu kura za kaunti pana ya Nairobi yenye wapiga kura zaidi ya milioni mbili.

Sifuna sasa anakuwa seneta wa tatu wa kaunti ya Nairobi tangu kuanzishwa kwa serikali za ugatuzi baada ya Mike Sonko ambaye baadae alikuja akawa gavana, Johnson Sakaja ambaye anawania ugavana wa kaunti hiyo ambaye matokeo ya kinyang'anyiro hicho yanatarajiwa kutangazwa muda mfupi ujao ambapo walikuwa wanamenyana kwa ukaribu na Poluycarp Igathe wa Jubilee.

Sifuna akizungumza baada ya kushinda useneta aliwashukuru wapiga kura wote waliojitokeza kwa wingi na pia kumshukuru Mungu kwa kumpa nafasi hiyo adimu ya kuingia kwenye seneti.