Johnson Sakaja ambwaga Igathe na kuwa gavana wa Nairobi

Polycarp Igathe wa Jubilee aliibuka wa pili kwa kura 573,516

Muhtasari

Polycarp Igathe wa Jubilee aliibuka wa pili kwa kura 573,516

Mgombea Ugavana wa Naairobi Johnson Sakaja mbele ya Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 15 2022.
Mgombea Ugavana wa Naairobi Johnson Sakaja mbele ya Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 15 2022.
Image: DOUGLAS OKIDY

Seneta wa Nairobi anayeondoka Johnson Sakaja ametangazwa kuwa gavana wa nne wa kaunti hiyo yenye wapiga kura zaidi ya milioni mbili.

Msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Nairobi, Albert Gogo alimtangaza Sakaja aliyekuwa akiwania kwa chama cha UDA kuwa mshindi baada ya kupata kura 699,392

Polycarp Igathe wa Jubilee aliibuka wa pili kwa kura 573,516.

Sakaja sasa anachukua kiti hicho kutoka kwa gavana anayeondoka Ann Kananu baada ya kuhudumu kwa takriban mwaka mmoja tangu alipochukua hatamu baada ya gavana Sonko kubanduliwa madarakani na bunge la kaunti.

Sonko alichukua kiti hicho kutoka kwa mfanyibiashara Evans Kidero ambaye ni gavaan wa kwanza tangu serikali za ugatuzi kuzinduliwa mwaka 2013.

Awali kulikuwepo na sintofahamu kuhusu uhalali wa Sakaja kuwania ugavana Nairobi baada ya kukumbwa na vita vikali vya uvumi uliosambazwa kwamba hakuwa na vyeti vya shahada ambacho ni kigezo kikubwa katika katiba kwa mtu kuwania ugavana lakini alipigana vikali uvumi huo na sasa ameibuka gavana wa kaunti ya Nairobi.

Johnson Sakaja hakuwepo katika ukumbi wa Kasarani kupokezwa cheti chake cha ushindi.

Kutangazwa kwa kura za viti vya useneta, ugavana na uwakilishi wa kike katika kaunti ya Nairobi kumechukuwa muda tangu mchakato mzima uanze kutokana na wingi wa wapiga kura katika kaunti hiyo pamoja pia na misukosuko ya wanasiasa kuzua vikali kutokana na kucheleweshwa kwa kutolewa kwa matokeo hayo.

Awali, Esther Passaris ambaye ni mwakilishi wa kike alikitetea kiti hicho kwa tikiti ya ODM na alionekana kweney kamera akimfokea vikali msimamizi wa uchaguzi Albert Gogo kwa kile wengi walisema ni kuteta kuhusu kucheleweshwa kwa matokeo hayo.