"Makamishna 4 waasi walitaka kulazimisha marudio ya uchaguzi wa urais" - Chebukati

Chebukati alisema makamishna hao walitaka kufanay hivyo kinyume na kiapo chao kuhudumu ofisini.

Muhtasari

• "Hii ni kinyume cha sheria kutaka kubadilisha haki ya wananchi wa Kenya,” Chebukati alinukuliwa

akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Image: ENOS TECHE

Vita baridi vinazidi kuimbuka tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC huku misukosuko ikizidi kutokota na nyufa kuonekana hata zaidi miongoni mwa makundi mawili ya makamishna wa tumwe hiyo.

Juzi kati baada ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kutangaza matokeo ya uchaguzi ambapo alimtawaza mpeperusha bendera wa Kenya Kwanza William Ruto kama mshindi, makamishna wanne kati ya saba wa tume hiyo walijitenga mbali na matokeo hayo katika kile walikitaja kuwa ni mkanganyiko wa kiza uliokumba takwimu za mkumbo wa mwisho kabisa wa matokeo hayo.

Makamishna hao waasi wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera waliitisha mkutano na wanahabari katika mgahawa wa Serena Nairobi sambamba na shughuli iliyokuwa ikiendelea Bomas Chebukati akitangaza matokeo.

Katika mkutano wao, Cherera na wenzake watatu walimshtumu Chebukati kwa kusema kwamab alikuwa na njama fiche ya kutanga kukoroga matokeo jambo ambalo walishindwa kuafikiana kama tume.

Kesho yake waliitisha mkutano tena katika hoteli hiyo na kumlimbikizia lawana mwenyekiti Chebukati kwa kusema kwamba hata takwimu hizo alizozitangaza zilikuwa zimezidi asilimia 100 na hivyo kujitenga mbali na matokeo hayo ambayo mshinde Raila Odinga pia aliyapuuzilia mbali na kudokeza kuelekea mahakamani kuyapinga.

Sasa Chebukati baada ya shutma hizo hatimaye Jumatano jioni alivunja ukimya wake na kuibua madai dhidi ya makamishna waasi kwamab walikuwa wanataka kuzibananga takwimu zile ili washindani wawili wakuu wapate asilimia sawa, hatua ambayo kikatibu ingelazimisha uchaguzi huo kurudiwa tena.

Chebukati aliwakashfu makamishna wa mrengo wa Cherera kwa kile alisema ni tamaa yao ya kutaka uchaguzi urudiwe kwa kukosekana mshindi kinyume na kiapo ambacho walitia wino wakati wanakula Yamini ya kuitumikia tume hiyo.

“Makamishna wanne, Juliana Cherera, Francis Wanderi, Justus Nyang’aya na Irene Masit walitaka kwamba mwenyekiti aboronge takwimu ili kuwezesha marudio ya uchaguzi, kinyume na kiapo chao cha kuhudumu kofisini. Hii ni kinyume cha sheria kutaka kubadilisha haki ya wananchi wa Kenya,” Chebukati alinukuliwa katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.