Patanisho: "Mke wangu aliniambia mimba aliyokuwa amebeba sio yangu" Jamaa aliyeachwa alipotoka kutazama mpira usiku adai

Mama ya Sharon hata hivyo hakuwa na habari njema kwa Jacob kwani alimwarifu kuwa Sharon kwa sasa ashapata mume mwingine na wanaishi naye Nairobi

Muhtasari

•Jacob alidai kuwa walikosana na mkewe wakati alienda kutazama mechi ya klabu ya Chelsea anayoshabikia na kukaidi agizo la mkewe aliyemtaka akae pale nyumbani.

•Mama Sharon pia alikana kuwa Jacob aliwahi kuwa mume wa binti yake na kudai kuwa walikuwa marafiki tu walipokuwa shuleni.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi jamaa aliyejitambulisha kama Jacob alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Sharon Akinyi ambaye walikosana mwaka wa 2019.

Jacob alidai kuwa walikosana na mkewe wakati alienda kutazama mechi ya klabu ya Chelsea anayoshabikia na kukaidi agizo la mkewe aliyemtaka akae pale nyumbani.

Isitoshe, Jacob ambaye ni mkaazi wa Kisumu alisema kuwa Sharon alimuarifu kuwa ujauzito aliokuwa amebeba sio wake.

"Nilienda kuangalia mechi ya Chelsea. Niliporudi kwa nyumba nikapata amenifungia mlango nikamuomba anifungulie kwani nilikuwa nimetoka tu kutazama mpira. Akaniuliza kwani mpira iliisha saa ngapi nami nikamwambia mahali nilienda kutazama mpira ni mbali..Alikasirika hadi hiyo siku nililala kwa rafiki yangu" Jacob alisema.

Jacob alisema kuwa alirudi kwa nyumba asubuhi iliyofuata na kumwarifu Sharon kuwa hawezi kosa kutazama mpira kwa sababu yake kwani yeye ni shabiki sugu wa Chelsea.

"Aliniambia hiyo pia ni sawa kisha akaniongelesha vibaya, siwezi sema kwa hewa nikamwekelea kofi. nilipoenda kazi keshowe nikapata ashaenda.. nilipompiga kofi aliniambia kuwa mimba aliyokuwa nayo sio yangu" Alisena Jacob.

Hata hivyo Sharon alipokuwa nyumbani kwa wazazi wake alimwarifu Jacob kuwa ujauzito aliokuwa amebeba ni wake na ni hasira tu zilikuwa zimemshinikiza kusema kuwa ni ya mwanaume mwingine.

Juhudi za Gidi kumfikia Sharon ili kumpatanisha na Jacob hazikufua dafu kwani aliyeshika simu ni mama ya Sharon.

Mama ya Sharon hata hivyo hakuwa na habari njema kwa Jacob kwani alimwarifu kuwa Sharon kwa sasa ashapata mume mwingine na wanaishi naye Nairobi.

Mama Sharon pia alikana kuwa Jacob aliwahi kuwa mume wa binti yake na kudai kuwa walikuwa marafiki tu walipokuwa shuleni.

"Sharon kwa sasa ako Nairobi na bwanake. Nilikwambia kuwa dadake alisema kuwa walipatana na mume mwingine huko Nairobi.. Ako na bwana yake" Mama Sharon aliambia Jacob.

"Huyo alikuwa rafiki yake wakati walikuwa wanasoma shuleni.. Hiyo mimba mimi sijui. Niliskia tu eti walipata mtoto na bwanake.. sijui kama mtoto ni wa Jacob" Mama Sharon aliarifu Gidi.

Jacob alisema kuwa walikuwa wamefunga ndoa na Sharon mwezi Oktoba 2018 ila hakuwa ameenda kujitambulisha kwa familia.

Je ushauri wako kwa Jacob ni upi?