"Ati wananiambia nimalize niende, kwani wanafikiria nimalize niende wapi?" - rais Kenyatta

Rais alizungumza wakati wa uzinduzi wa hospitali iliyojengwa na NMS.

Muhtasari

• Alisema mrengo wa naibu wake umejawa na matusi ambao kila mara wanamsema yeye.

• Aidha, rais Kenyatta alidokeza kwamba hata akimaliza hakuna mahali ataenda kwa sababu atakuwa tu bado.

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta
Image: State House Kenya (Facebook)

Raia Uhuru Kenyatta kwqa mara nyingine amezua mjadala mitandaoni baada ya kusikika akizungumza kwamba hata kama atamaliza muhula wake kushika hatamu kama rais, haendi popote kwani atakuwa hapa bado.

Akizungumza jana katika eneo bunge la Kasarani Mwiki ambapo alikuwa anazindua hospitali iliyojengwa na mamlaka ya jiji kuu la Nairobi, NMS, rais Kenyatta alionekana kuwapigia debe kinara wa Azimio-One Kenya Raila Odinga na mgombea mwenza Martha Karua huku akisema kwamba hao ndio mpango mzima na hao wengine – kwa maana ya naibu rais na mrengo wake ni watu wa matusi.

“Mama ambaye hacheki anaitwa Martha Karua, hawa ni watu ambao wanasimama na ni wa haki, niseme ukweli bwana, hawa wengine ni wa mdomo na matusi. Sasa mimi nauliza ukiwaona kila siku wanaenda kwa mkutano ni kuongea juu ya Uhuru, na Uhuru hatafuti kura. Ati wananiambia nimalize niende, kwani wanafikiria nimalize niende wapi, si nitakuwa hapa tu,” rais Kenyatta alihutubia umati uliokuwa ukimshangilia.

Rais Kenyatta alisisitiza maneno yake kwamba atafanya kazi yake mpaka dakika ya mwisho bila kushrutishwa na mtu yeyote kwani yeye ndiye mkuu wa majeshi kwa sasa.

Alisema bado kuna miradi mingi ya kufanywa na serikali mpaka atakapomkabidhi mwingine nafasi hiyo huku akiwataka watu kwac heshima kubwa kumchagua Raila Odinga kama rais wa kumrithi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Nawaomba ninyi kwa heshima, kwamba yule ambaye nitapatia aendelee iwe si mwingine bali Raila Odinga,” rais Kenyatta alisema.

Rais Kenyatta amekuwa katika siku za hivi karibuni akionesha kutofautiana na naibu wake William Ruto hadharani huku wawili hao ambao kwa wakati mmoja walikuwa marafiki wakubwa wa kufananisha mpaka nguo wakitupiana cheche kali.

Wiki jana wakati wa mahojiano ya moja kwa moja na kujibu maswali ya wananchi, Ruto alidai kwamba rais Kenyatta ndiye aliyechangia pakubwa mgawanyiko wao huku akimshtumu kwa kukataa wito wa maaskofu na viongozi wa kanisa waliotaka kuwapatanisha na kurejesha amani na urafiki wao.