Mundigi: Mkulima mdogo aliyewabwaga mabwenyenye na kushinda Useneta Embu

Aliwaangusha gavana Wambora na seneta Ndwiga ambao wote walikuwa wanawania useneta Embu.

Muhtasari

• Mundigi aliwarambisha sakafu gavana anayeondoka Martin Wambora, seneta wa sasa Peter Ndwiga miongoni mwa majina tajika waliokuwa wakiwania useneta Embu.

Seneta mteule wa Embu, Alexender Munyi Mundigi
Seneta mteule wa Embu, Alexender Munyi Mundigi
Image: Alexendar Munyi Mindigi//Facebook

Mkulima Alexender Mundigi aliwashangaza wengi katika uchaguzi uliopita baada ya kushinda uchaguzi wa useneta katika kaunti ya Embu kupitia tikiti ya chama cha DP.

Mundigi ambaye ni mkulima mwenye mtaji mdogo aliwashangaza wengi baada ya kusemekana kwamba hakutumia pesa na magari ya kifahari katika kampeni zake kama ambavyo washindani wake walikuwa wanafanya kampeni kwa njia ya kifahari bali yeye alikuwa anazunguka tu kutafuta kura kutokana na michango midogo midogo kutoka kwa wasamaria wema.

Kilishowaacha wengi katika mshangao mkubwa ni jinsi mkulima huyo mwenye kipato cha kadri aliwabwaga wanasiasa weney majina makubwa akiwemo gavana wa sasa anayeondoka Martin Wambora aliyekuwa akiwania useneta baada ya kipindi chake cha miaka kumi kama gavana kukamilika kikatiba.

Mundigi alipata kura 81,162, akimshinda mpinzani wake wa karibu, naibu gavana anayeondoka David Kariuki ambaye aliwania kwa tikiti ya UDA na kupata 55,695 huku Lilian Mbogo ambaye kwa wakati mmoja aliwahi kuhudumu kama katibu mkuu wa vijana akiibuka wa tatu na kura 22,851 kupitia chama cha Jubilee.

Seneta wa sasa Peter Ndwiga aliibuka wa tano kwa kura 17,11 huku Gavana Wambora ambaye pia alikuwa akikimezea mate kiti hicho alibwagwa hadi nafasi ya tano kwa kura 13,523 tu!

Mundigi, seneta mteule, alipiga kampeni zake katika kaunti ya Embu akiwa na gari moja tu lililobandikwa mabango yake, tofauti na washindani wake, ambao walikuwa na mabango kote kaunti ya Embu na mabango ya kuvutia, Mundigi hakuwa na bango hata moja lakini aliibuka kidedea.