Kigame awataka wafuasi wake kumpigia kura kwa kuandika jina lake kwenye karatasi za kura

Alisema IEBC ilimkosea kumtema nje ya kipute cha urais.

Muhtasari

“Sio kura iliyoharibika, ingawa wataiita hivyo. Ni kura yetu ya fahari, ya kidemokrasia dhidi ya udhalimu!" - Reuben Kigame.

Mgombea urais Reuben Kigame akihutubia wanahabari nje ya jumba la Anniversary Tower Nairobi, baada ya jaribio lake kukutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kugonga mwamba./WILFRED NYANGARESI
Mgombea urais Reuben Kigame akihutubia wanahabari nje ya jumba la Anniversary Tower Nairobi, baada ya jaribio lake kukutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kugonga mwamba./WILFRED NYANGARESI

Mwinjilisti na mwanasiasa Reuben Kigame bado anaonekana kutokana tamaa katika azma yake ya kuwa mrithi wa rais Kenyatta, hata baada ya tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC  kumfungia nje ya kinyang’anyiro hicho kwa kukosa kuafikia vigezo fulani.

Kigame sasa anawataka wafuasi wake kuwa na Imani kwamba yeye ndiye chaguo bora na kumchagua kama rais licha ya jina lake kukosekana kwenye karatasi za kupiga kura hapo Agosti 9 ambayo ni kesho.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Kigame amewapa wafuasi wake njia mbadala jinsi watakavyofanikisha kuchaguliwa kwake kama rais na amewahakikishia kwamba mbinu hiyo itazaa matunda.

“Jinsi ya kumpigia kura Reuben Kigame kama rais:

  1. Piga kura kwa fahari kwa MCA, Mbunge, WRP, Gavana na Seneta wako.
  2. Ukiwa na tabasamu kubwa usoni, chagua kura ya urais, andika jina ‘Reuben Kigame’ na kalamu yako kama chaguo la tano, liweke tiki na liweke kwenye kisanduku sahihi,” Kigame aliwarai wafuasi wake.

Alizidi kusema kwamba kwa hakika kura hiyo haitahesabiwa kama yenye imeharibika hata ingawa baadhi ya maafisa watakaosimamia uchaguzi huo wataiita hivyo. Aliwaambia kwamba hizo karatasi za kupiga kura zimelipiwa na wakenya kutoka kwa ushuru wao wenyewe na hivyo hawafai kutebwereka nyumbani bure kwamba hayuko kwenye karatasi za kura kwa hiyo hawana haja ya kutoka kuenda kupiga kura.

“Sio kura iliyoharibika, ingawa wataiita hivyo. Ni kura yetu ya fahari, ya kidemokrasia dhidi ya udhalimu! Tumelipia karatasi za kupigia kura kwa kodi zetu hata hivyo, kwa hivyo tuzitumie. Usikae nyumbani! Yeyote anayelalamika, wakumbushe IEBC iliomba, na huu ni mwanzo tu.. Aluta continua!” aliandika Kigame.

Awali baada ya IEBC kumfungia nje ya kinyang’anyiro cha urais, Kigame na timu yake walielekea katika mahakama kuu ambapo kesi yao ilifaulu na jaji Anthony Mrima alisema yalikuwa ni makosa kwa IEBC kumfungia nje ila akakataa kuiamuru IEBC kuliongeza jina lake kwani muda ulikuwa umeyoyoma. IEBC iliteta kwamba kuliongeza jina lake kwenye karatasi za kupiga kura kutahitaji hela zingine zaidi na hivyo kukiuka bajeti yao.