UDA ya Ruto Yaramba Nyadhifa Nyingi Katika Eneo Bunge la Nyumbani kwa PS Kibicho

Eneo bunge hilo lilikuwa na jumla ya wapiga kura 69,743 waliojiandikisha.

Muhtasari

• GK aliwashinda washindani wake wengine sita huku Wasusana Mark Mithamo akiibuka wa pili kwa kura 13,083. Elphas Kangangi wa Jubilee alifanikiwa kura 5,419.

Mbunge mteule wa Ndia George Kariuki akionyesha cheti chake baada ya kutangazwa kuwa mbunge wa eneo bunge hilo.
Mbunge mteule wa Ndia George Kariuki akionyesha cheti chake baada ya kutangazwa kuwa mbunge wa eneo bunge hilo.
Image: WANGECHI WANG'ONDU

CHAMA cha Naibu Rais William Ruto cha UDA kimejishindia nyadhifa nyingi katika eneo la Mlima Kenya eneo bunge la Ndia. Ndia ni eneo bunge analoishi katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Karanja Kibicho.

Mbunge wa sasa George Kariuki almaarufu G.K alichaguliwa tena kwa jumla ya kura 25,031 kati ya 48,393 zilizopigwa katika uchaguzi wa Jumanne.

GK aliwashinda washindani wake wengine sita huku Wasusana Mark Mithamo akiibuka wa pili kwa kura 13,083. Elphas Kangangi wa Jubilee alifanikiwa kura 5,419.

Msimamizi wa uchaguzi wa eneo bunge hilo Francis Njogu pia alitangaza na kuwasilisha vyeti kwa MCAs watatu waliochaguliwa katika eneo bunge hilo ambao walishinda kwa tikiti za UDA.

Walikuwa ni MCA wa wadi ya Kariti mteule Kariuki Jeremiah Makimi aliyepata kura 5,934, mteule wa wadi ya Kiini Gakuru Geoffrey Murimi aliyesimamia kura 7,268 na Thomas Mwangi Muriuki wa wadi ya Mukure aliyeshinda kwa kura 6,475.

Wakizungumza baada ya kupokea vyeti vyao viongozi hao wanne waliochaguliwa wamewashukuru wapiga kura kwa kuweka imani yao katika uwezo wao wa kutoa uongozi bora huku wakiahidi kutowaangusha.

Aidha, waliwataka washindani wao kuungana na kufanya kazi pamoja katika azma ya kuwawezesha wakazi wa Ndia.

Mbunge mteule George Kariuki aliahidi kuongeza kasi katika muhula wa pili wa huduma kwa wapiga kura wake.

"Napenda kuwashukuru kwa kunichagua tena kwa muhula wa pili. Naahidi kuwafanyia kazi ipasavyo wote pamoja na kuboresha utoaji huduma katika kipindi changu cha pili," aliongeza.

Kulingana na data ya pamoja ya IEBC, Naibu Rais William Ruto aliongoza katika eneo bunge hilo kwa kujizolea jumla ya kura 41,293 dhidi ya mgombea urais wa Azimio One Kenya Raila Odinga aliyeibuka wa pili kwa jumla ya kura 6,873.

Mgombea wa Seneta wa UDA James Kamau Murango alishinda katika eneo bunge hilo kwa kujizolea kura 35,900 dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Jubilee Daniel Karaba aliyepata kura 5,968.

Jane Njeri ambaye aliwania kiti cha uwakilishi mwanamke kwa tiketi ya UDA aliongoza kwa kura 33,804 dhidi ya Shujaa Rose Wachira wa Jubilee aliyepata kura 7,599.

Eneo bunge hilo lilikuwa na jumla ya wapiga kura 69,743 waliojiandikisha.