Upigaji Kura Ungali Kufanyika Eldas Wajir Licha ya IEBC Kutoa Agizo

Wakazi wanasema wana wasiwasi kuwa yaliyotokea jana yatajirudia leo, na hawataweza kupiga kura.

Muhtasari

• Wakazi wanasema wana wasiwasi kuwa yaliyotokea jana yatajirudia leo, na hawataweza kupiga kura.

Wapiga kura wakivamia lango la Moi avenue.
Wapiga kura wakivamia lango la Moi avenue.
Image: SUSAN MUHINDI

Uchaguzi mkuu ulifanyika Jumanne Agosti 9 kote nchini ila kuna baadhi ya sehemu zililazimika kuahirisha chaguzi kufuatia mkanganyiko wa vifaa vya uchaguzi na sehemu zingine zikikumbwa na vurugu.

IEBC ilitoa taarifa kwamab chaguzi hizo zilizoahirishwa kutokana na vurugu au mikanganyiko zingefanyika Jumatano, ila sasa taarifa zinaarifu kwamba licha ya agizo hilo bado uchaguzi ungali haujaanza katika eneo bunge la Eldas kaunti ya Wajir, uchaguzi ambao ulitatizwa baada ya milio ya risasi kusikika katika ukumbi wa CDF huko Eldas na watu kutawanyika miguu niponye.

Mpaka Jumatano asubuhi, wapiga kura wenye matumaini ya kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia kuwachagua viongozi wao walikuwa bado kwenye foleni licha ya shughuli yoyote kuonekana kutoendelea.

Hata hivyo, afisa aliyehusika aliondoa uvumi kwamba kulikuwa na matatizo ya usalama, lakini akasema usafirishaji wa masanduku ya kura hadi vituo vya kupigia kura ni tatizo kubwa.

Wakazi wanasema wana wasiwasi kuwa yaliyotokea jana yatajirudia leo, na hawataweza kupiga kura.

Uchaguzi huo ulikuwa umeahirishwa pia katika sehemu mbalimbali kama vile ugavana kaunti ya Mombasa, ugavana kaunti ya Kakamega na ubunge katika maeneo ya Pokot.

Tume huru ya mipaka na uchaguzi iliweka wazi kwamba chaguzi hizo zingeendelea Jumatano huku sehemu ambazo kura zilipigwa tayari matokeo ya awali yakianza kutolewa kwa idadi ya jinsi kura hizo zilivyopigwa.