"Odinga akubali matokeo ama historia imkumbuke kama mtu mwenye tamaa ya madaraka"

Maneno hayo yalitolewa na kiongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Julius Malema.

Muhtasari

• Julius Malema alimtaka Odinga kutokuwa sehemu ya utamaduni wa kusababisha ukosefu wa utulivu, na kutokuwa na uhakika juu ya utawala wa Afrika

Kiongozi wa upinzani wa South Africa amemtaka Odinga kukubali matokeo ya uchaguzi
Julius Malema, Railac Odinga Kiongozi wa upinzani wa South Africa amemtaka Odinga kukubali matokeo ya uchaguzi
Image: Twitter, maktaba

Kiongozi wa muda mrefu wa mrengo wa upinzani katika Jamhuri ya Afrika Kusini Julius Malema amechukizwa na hatua ya kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kuwasilisha ombi katika mahakama ya upeo kupinga kutangazwa kwa William Ruto kama rais mteule wa Kenya.

Kupitia ukurasa wa Twitter, kinara huyo wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters alimtaka Odinga kukubali matokeo na kujiunga na walioshinda kusukuma gurudumu la maendeleo mbele na kumuonya kwamba kuendelea kwake kupinga matokeo kila mara baada ya uchaguzi kutaifanya historia ya taifa la Kenya kumhukumu vibaya tena kwa njia hasi.

Malema alisema Raila ni kiongozi shupavu ambaye ameipigania nchi ya Kenya katika mengi mazuri lakini hatua yake ya kutokubali matokeo ya kila baada ya uchaguzi itamletea historia ya kuwa mtu aliyekuwa anahaha na kuhangaika juu chini kupata uongozi huku akiteketeza jitihada za taifa kutaka kusonga mbele kimaendeleo.

“Bw Odinga lazima anyenyekee, na kukubali matokeo na pia kuingia katika sehemu ya serikali ambayo itashughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Kenya, na kutoruhusu historia kumkumbuka kama mtu ambaye alikuwa na tamaa ya madaraka, kwa gharama ya maendeleo ya taifa lake,” Malema alisema kupitia ukurasa rasmi wa chama cha EFF.

Kulingana na Malema, Raila amepigana sana na ni muda kukubali matokeo ili kuzuia mtafaruku na mvurugano ambao utasababishwa na wafuasi wake kwa hatua yake ya kutokubaliana na matokeo.

“Tunatoa wito kwa Bw. Raila Odinga kukubali matokeo ya uchaguzi, na sio kuwa sehemu ya utamaduni wa kusababisha ukosefu wa utulivu, na kutokuwa na uhakika juu ya utawala wa Afrika,” chama hicho kilimnukuu Malema.

Wiki jana tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilimtangaza naibu rais anayeondoka William Ruto kama rais mteule na kumbwaga Odinga kwa kura chache.

Ruto alikuwa anawania urais kwa mara yake ya kwanza kabisa huku kwa upande mwingine Odinga ilikuwa mara yake ya tano kuwania urais na kupoteza.