Bottom-Up: Jamaa aliyekuwa Muuza Mkaa Ateuliwa Mbunge Kuresoi North

Mutai Alfred alikuwa anachoma na kuuza mkaa akiwa kidato cha kwanza na kujilipia karo

Muhtasari

• Alielezea kwamba kwa wakati mmoja aliwahi shikwa na polisi na kupandishwa kizimbani kwa kosa la kuharibu mazingira.

Mwanasiasa Mutai Alfred
Mwanasiasa Mutai Alfred
Image: Facebook//MutaiAlfred

Alfred Mutai ndiye mbunge mpya wa eneo bunge la Kuresoi Kaskazini baada ya kujinyakulia ushindi mnono wa kura zipatazo zaidi ya elfu 25 kupitia tikiti ya chama cha UDA.

Mutai ambaye awali alihudumu kama mjumbe wa kaunti ya Nakuru akiwakilisha eneo dogo la Sirikwa kando na kuwa katika siasa, maisha yake ya awali ni jambo la kuzungumziwa na kutia moyo sana kwa wakati mmoja.

Inasemekana kwamba mbunge huyo mpya kabisa katika tovuti za bunge aliwahi kushiriki katika kitendo haramu cha uchomaji mkaa mapema miaka ya 2000 akiwa kidato cha kwanza, kutokana na ugumu wa maisha, Mutai alishiriki biashara hiyo ya magendo ili kujikimu kupata karo.

“Kumpoteza mzazi katika umri mdogo haikuwa rahisi. Ilinilazimu kufanya kazi katika umri mdogo ili kuungana na ndugu zangu wakubwa kusaidia wengine na pia ili (nipate) pesa za karo yangu ya shule, lakini kwa bahati nzuri nilimaliza masomo yangu baada ya kuhangaika sana,” aliiambia jarida moja la humu nchini katika mahojiano ya awali.

Mwanasiasa huyo ambaye maisha yake ni mfano halisia wa methali na misemo mingi inayozungumzia kubadilika kwa maisha kutoka umaskini hadi utajiri katika mahojiano hayo alikumbuka kisa kimoja ambapo alitiwa mbaroni na kufikishwa mahakama ndogo ya Molo kushtakiwa dhidi ya kuuza mkaa kinyume cha sheria.

“Nilijua biashara ilikuwa haramu lakini sikuwa na mbadala. Nilihitaji kwenda shule mimi mwenyewe na ndugu zangu pia walikuwa wakisoma, lakini namshukuru hakimu kwa kunisikiliza wakati wa kupunguza kabla ya kuhukumiwa," alieleza Mutai kwenye mahojiano.

Mwanasiasa huyo pindi baada ya kutangazwa mshindi katika eneo bunge hilo, alimshukuru Mungu na kuwashukuru wananchi wote waliojitokeza kwa idadi kubwa kumuaminia katika kuwawakilisha na majukumu yao bungeni.