Akiwa Mafichoni, Didmus Barasa Amewashukuru Watu wa Kimilili Kwa Kumchagua Tena

“Asanteni sana wananchi wa jimbo la kimilili kwa kunichagua tena kwa kishindo kwa muhula mwingine. - Didmus

Muhtasari

“Asanteni sana wananchi wa jimbo la kimilili kwa kunichagua tena kwa kishindo kwa muhula mwingine." - Didmus Barasa.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: Facebook//DidmusBarasa

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amejipa hongera kufuatia ushindi wake mkubwa kutetea wadhfa wake huo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne.

Mbunge huyo ambaye yuko mafichoni baada ya kudaiwa kumpiga risasi na kumuua mlinzi wa mshindani wake Brian Khaemba aliyekuwa anagombea kwa tikiti ya chama kipya kabisa nchini DA-K.

Barasa alikitetea kiti chake hicho kwa tikiti ya chama cha UDA ambapo alitangazwa mshindi wa kinyang'anyiro cha Kimilili Jumatano usiku baada ya kujizolea kura 26, 861 na kuwabwaga chini washindani wake watatu.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Didmus Barasa alijipa hongera huku akiwashukuru wapiga kura kwa kumuaminia na kumchagua.

“Asanteni sana wananchi wa jimbo la kimilili kwa kunichagua tena kwa kishindo kwa muhula mwingine. Nawapenda kwa vipande,” Barasa aliandika kwenye ukurasa wake.

Thank you the great people of KIMILILI CONSTITUENCY for re-electing me overwhelmingly for another term. I LOVE YOU TO BITS❤️ #KimililiPeopleFirst #TunaendeleaNaKazi

Posted by Didmus Barasa on Wednesday, August 10, 2022

Sasa hili linazidi kuleta mkanganyiko zaidi huku akiwa bado yupo mafichoni baada ya kisa hicho kilichotokea Jumanne usiku na mpaka sasa licha ya kutakiwa na vyombo vya dola kujitokeza na kuandikisha ripoti bado hajaridhia.

Jumanne, mkuu wa kitengo cha upelelezi wa jinai nchini Kenya, DCI wa Bungoma Joseph Ondoro alisema Barasa alizozana na Khaemba, hatua ambayo ilimfanya  mpinzani huyo wake kuondoka na kuelekea kwenye gari lake.

"Barasa alimfuata akiwa na wanaume wanne na kuwaamuru wasimruhusu (Khaemba) kuondoka mahali hapo lakini dereva wa Khaemba Joshua Nasokho alikaidi amri hiyo na kuwasha gari," alisema Ondoro.

 

Hapo ndipo Barasa alipochomoa bastola na kumlenga msaidizi wa Khaemba Brian Olunga na kumpiga risasi ya paji la uso.Olunga alifariki katika hospitali ya Kimilili Subcounty alipokuwa anapokea matibabu ya dharura.

Sasa watu wameibua madai mengi kuhusu uwezo na utayarifu wa vyombo vya sheria kumwajibisha mbunge huyo kwani mpaka sasa bado yupo mafichoni na silaha aliyoitumia ingali bado kusalimishwa na sasa inaonekana ana uwezo wa kufikia mitandao ya kijamii mpaka kupakia na kufuatilia matukio ya uchaguzi na taasisi husika zingali bado kumweka chini ya ulinzi.

Kinachoshindikana ni kipi?