CEO wa Sportpesa Ronald Karauri ashinda ubunge Kasarani kama mgombea huru

Ahsante sana watu wa Kasarani na kwa kweli mmeniheshimisha kwa kura zenu - Karauri.

Muhtasari

• "Tumevunja rekodi, mimi ndiye mgombea binafsi wa kwanza kuchaguliwa Nairobi." - Karauri.

Mkurugenzi mtendaji wa Sportpesa, Ronald Karauri
Mkurugenzi mtendaji wa Sportpesa, Ronald Karauri
Image: Facebook//RonaldKarauri

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ubashiri ya SportPesa Ronald Karauri ametangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa eneo bunge la Kasarani, jijini Nairobi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alipata kura 32,406 akifuatiwa kwa karibu na mpinzani wake John Njoroge aliyepata kura 30,444. Afisa wa IEBC alisema kuwa jumla ya wapiga kura katika eneo bunge hilo ni 155,405.

Karauri aliwania kiti cha ubunge kama mgombeaji huru na anachukua nyqadhifa hiyo  kutoka kwa mbunge wa sasa Mercy Gakuya wa chama cha Jubilee.

Wakati wa uteuzi wa chama, aliazimia kujiunga na Jubilee lakini akashindwa kwenye kura ya mchujo na kuamua kuwa mgombeaji huru.

Katika hotuba yake ya kukubalika, alisema kuwa watu wa Kasarani wamemsaidia kuvunja rekodi.

"Tumevunja rekodi, mimi ndiye mgombea binafsi wa kwanza kuchaguliwa Nairobi. Ahsante sana watu wa Kasarani na kwa kweli mmeniheshimisha kwa kura zenu, mimi si jamaa asiyedanganya na vile vitu nimeahidi vyote nitafanya na nitatimiza na mnajua hilo." alisema.

Aliongeza kuwa atafurahi kufanya kazi pamoja na watu wa Kasarani ili kufanikisha mambo.

Ushindi wa Karauri unakuja huku taifa likiingia siku ya pili ya uhesabu wa kura katika nyadhifa mbalimbali na baadhi ya sehemu ambako kumekamilika taayri washindi wakiwa wameanza kutangazwa na sherehe kuanza kurindimwa.